Thursday, October 25, 2012

WANANCHI WANAHAMASISHWA KUCHANGIA DAMU KWA HIARI KUOKOA MAISHA YA WAGONJWA WANAOHITAJI DAMU HOSPITALINI

  Kutoka http://www.issamichuzi.blogspot.se/2012/10/wananchi-wanahamasishwa-kuchangia-damu.html
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Mh. Leonidas Gama akichangia katika kituo cha damu salama Kilimanjaro siku ya ijumaa tarehe 19/10/2012 hii ni mara ya pili mwaka huu kwa Mheshimiwa Gama kuchangia baada ya kuchangia mwezi juni 2012 wakati wa maadhimisho ya siku ya wachangia damu duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoani hapo. 

Mpango wa Taifa wa Damu salama Unatoa WITO kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu kwa hiari kwenye vituo vya damu salama 
Damu ni Uhai na inahitajika, mahitaji ya damu nchini ni wastani wa chupa 400,000 kwa kipindi cha oktoba 2011- Septemba 2012 mpango umekusanya chupa 110,000.
Upungufu wa damu katika vituo vya damu salama husababisha wagonjwa kupoteza maisha kwa kukosa damu au kutopata damu kwa wakati, vifo ambavyo vinaweza zuilika kama watanzania watajenga utamaduni wa kuchangia damu mara kwa mara
Upungufu wa damu unatokana na sababu zifuatazo;
  • Uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari
  • Kuenea kwa maambukizi ya ukimwi, hivyo kusababisha watu kuwa waoga kuchangia damu
  • Uuzwaji wa chupa za damu mahospitalini kunakofanywa na watumishi wasio waaminifu hivyo kukatisha watu tama
  • Imani potofu katika jamii kuhusu uchangiaji damu Mfano uchangiaji damu unaweza kusababisha kupata maambukizi kitu ambacho si kweli
Wananchi wanaombwa kutembelea vituo vifuatavyo kuchangia damu;
 Mwanza- karibu na Hospitali ya Bugando
Tabora – karibu na Hospitali ya kitete
Dar-es-salaam- ilala mchikichini, hospitali ya lugalo, kituo kidogo cha mnazi mmoja
Mbeya- karibu na Hospitali ya Meta
Kilimanjaro- Karibu na Hospitali KCMC
Mtwara- karibu na Hospitali ya Ligula
Lindi- kituo kidogo karibu na uwanja wa ilulu
Dodoma – kituo kidogo nje ya Hospitali ya mkoa (Jenero)
Morogoro- Kituo kidogo karibu na Hospitali ya mkoa
Kagera- kituo kidogo
Na Hospitali nyingine yoyote ambayo inatoa huduma ya kuongeza damu
Kwa maelezo zaidi piga simu namba 0222181873 au 0712612000
Kumbuka; Inawezekana damu unayochangia ni kwa ajili yako, familia na jamii

Thursday, October 11, 2012

SERIKALI NA TIB ZATILIANA SAINI MKATABA WA UJENZI WA SOKO LA KIMATAIFA KILIMANJARO

 

Kutoka  MUHIDIN MICHUZI


Na Dixon Busagaga wa globu ya jamii,Moshi.


SERIKALI mkaoni Kilimanjaro na Benki ya uwekezaji nchini (TIB) zimetiliana saini ya mkataba wa mkopo wa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa la mazao ya nafaka la Lokolova, ikiwa ni hatua za awali zenye lengo la kuimarisha soko la bidhaa za ndani.



Zoezi hilo la utiaji saini lilifanywa na katibu tawala wa mkoa wa Kilimanjaro(RAS) Faisal Issa na mwakilishi wa wa benki ya TIB ,Allan Magoma katika ofisi za mkuu wa mkoa na kushuhudiwa na waziri wa jumuiya ya Afrika Mashariki Samwel Sitta, na mkuu wa mkoa Leonidas Gama .



Akizungumza mara baada ya zoezi hilo waziri Sitta alipongeza jitihada za mkoa wa Kilimanjaro, za kutafuta fedha za ujenzi wa soko hilo, ambalo litaweza kuongeza bei ya bidhaa za ndani zinazouzwa katika nchi
wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.



Waziri Sitta alisema katika shughuli za biashara kuwa na masoko ya uhakika kutasaidia kuondoa ulanguzi uliopo, na kuongeza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuigwa na mikoa mingine kulingana na fursa zilizopo.



Alisema mkoa wa Kilimanjaro umekuwa na bahati kubwa ya kupata mkopo ambao utasaidia kuongeza tija kwa wananchi ikiwemo kukuza mapato, ya mwananchi mmoja mmoja, mkoa na taifa kwa ujumla.



Pia alisema ni wajibu wa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro kuanza kubuni mipango ya matumizi sahihi ya soko hilo ili kuleta faida kwa Tanzania, ikiwemo uuzaji wa mazao yenye viwango na ubora wa kimataifa, ili
kumudu ushindani.



Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alisema mchakato wa uanzishwaji wa soko hilo ulizingatia mahitaji na fursa za kiuchumi ambazo kwa kiasi kikubwa zina mchango kwenye kukuza pato la mkoa na taifa.



Gama alisema kwa kipindi cha mwezi Machi mpaka Julai mwaka huu pekee, serikali na wananchi wameweza kunusuru mapato makubwa ambayo yalikuwa yanapotea kutokana na wafanyabiashara kuuza mazao ya nafaka nje ya nchi kwa njia za magendo.



Kwa mujibu wake Gama, soko hilo la muda la himo, limeweza kuvusha jumla ya tani 26,585 zilizowezesha mamlaka ya mapato (TRA) kupata jumla ya dola za kimarekani 30,072 sawa na shilingi milioni 45, huku
halmashauri ya wilaya ya Moshi ikipata milioni 80 na halmashauri ya wilaya ya Rombo ikipata jumla ya shilingi milioni 21.176,.



Ujenzi wa soko hilo unazingatia maeneo kwa ajili ya maegesho, maghala ya kuhifadhi nafaka na kuwa na mashine zitakazotumika kuchambua nafaka na kuzifunga kwenye vipimo maalum tayari kusafirishwa kwenda nchi mbali mbali za Afrika Mashariki na kati.