Thursday, October 11, 2012

SERIKALI NA TIB ZATILIANA SAINI MKATABA WA UJENZI WA SOKO LA KIMATAIFA KILIMANJARO

 

Kutoka  MUHIDIN MICHUZI


Na Dixon Busagaga wa globu ya jamii,Moshi.


SERIKALI mkaoni Kilimanjaro na Benki ya uwekezaji nchini (TIB) zimetiliana saini ya mkataba wa mkopo wa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa la mazao ya nafaka la Lokolova, ikiwa ni hatua za awali zenye lengo la kuimarisha soko la bidhaa za ndani.



Zoezi hilo la utiaji saini lilifanywa na katibu tawala wa mkoa wa Kilimanjaro(RAS) Faisal Issa na mwakilishi wa wa benki ya TIB ,Allan Magoma katika ofisi za mkuu wa mkoa na kushuhudiwa na waziri wa jumuiya ya Afrika Mashariki Samwel Sitta, na mkuu wa mkoa Leonidas Gama .



Akizungumza mara baada ya zoezi hilo waziri Sitta alipongeza jitihada za mkoa wa Kilimanjaro, za kutafuta fedha za ujenzi wa soko hilo, ambalo litaweza kuongeza bei ya bidhaa za ndani zinazouzwa katika nchi
wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.



Waziri Sitta alisema katika shughuli za biashara kuwa na masoko ya uhakika kutasaidia kuondoa ulanguzi uliopo, na kuongeza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuigwa na mikoa mingine kulingana na fursa zilizopo.



Alisema mkoa wa Kilimanjaro umekuwa na bahati kubwa ya kupata mkopo ambao utasaidia kuongeza tija kwa wananchi ikiwemo kukuza mapato, ya mwananchi mmoja mmoja, mkoa na taifa kwa ujumla.



Pia alisema ni wajibu wa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro kuanza kubuni mipango ya matumizi sahihi ya soko hilo ili kuleta faida kwa Tanzania, ikiwemo uuzaji wa mazao yenye viwango na ubora wa kimataifa, ili
kumudu ushindani.



Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alisema mchakato wa uanzishwaji wa soko hilo ulizingatia mahitaji na fursa za kiuchumi ambazo kwa kiasi kikubwa zina mchango kwenye kukuza pato la mkoa na taifa.



Gama alisema kwa kipindi cha mwezi Machi mpaka Julai mwaka huu pekee, serikali na wananchi wameweza kunusuru mapato makubwa ambayo yalikuwa yanapotea kutokana na wafanyabiashara kuuza mazao ya nafaka nje ya nchi kwa njia za magendo.



Kwa mujibu wake Gama, soko hilo la muda la himo, limeweza kuvusha jumla ya tani 26,585 zilizowezesha mamlaka ya mapato (TRA) kupata jumla ya dola za kimarekani 30,072 sawa na shilingi milioni 45, huku
halmashauri ya wilaya ya Moshi ikipata milioni 80 na halmashauri ya wilaya ya Rombo ikipata jumla ya shilingi milioni 21.176,.



Ujenzi wa soko hilo unazingatia maeneo kwa ajili ya maegesho, maghala ya kuhifadhi nafaka na kuwa na mashine zitakazotumika kuchambua nafaka na kuzifunga kwenye vipimo maalum tayari kusafirishwa kwenda nchi mbali mbali za Afrika Mashariki na kati.

No comments:

Post a Comment