Thursday, July 12, 2012
Rehema Matowo,Same
UHARIBIFU wa mazingira, watendaji wa Serikali kutojua umuhimu wa ufugaji nyuki na ukosefu wa vifaa bora vya ufugaji, zimetajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazokwamisha jitihada za wafugaji wa nyuki wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Hayo yaisemwa jana na Mratibu wa asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na masuala ya kilimo endelevu wilayani humo, Samwel Mdungu, alipokuwa akizungumza katika warsha ya kimataifa kuhusu ufugaji nyuki iliyohusisha washiriki kutoka nchi za Gambia, Zambia, Kenya Uganda na wenyeji Tanzania .
Mdungu alisema lengo la warsha hiyo ni kutafuta mbinu zitakazowawezesha wafugaji kuendeleza ufugaji nyuki utakaowawezesha kujipatia vipato vyao na na taifa kwa jumla.
Mratibu huyo alisema licha ya wananchi kuwa na mwamko wa ufugaji nyuki, bado kuna changamoto kubwa inayotokana na wananchi kuchoma misitu, jambo linalosababisha nyuki kuhama.
Hali kadhalika, watendaji wa Serikali kutoona umuhimu wa kuhamasisha ufugaji nyuki na wafugaji kutokuwa na vifaa vya kujikinga wakati wa kurina asali.
“Wenzetu wa Zambia wako mbali kwenye ufugaji nyuki na ndio maana tuko nao hapa ili waweze kutufundisha jinsi ya kutega nyuki, kutengeneza mizinga ya kisasa na mkutano huu utasaidia wafugaji wetu kupata masoko ya nje ya kuuzia bidhaa zao,”alisema Mdungu.
Akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi, alisema lengo la warsha hiyo ni kuwawezesha wafugaji nyuki kupata elimu ya ufugaji itakayowasaidia wao na familia zao, kujikwamua kiuchumi.
Alisema bado ufugaji nyuki unadharauliwa na kuoneka kuwa hauna tija jambo ambalo sio kweli .
Alisema kwa kipindi atakachokuwa mkuu wa wilaya kwenye wilaya hiyo, atahakikisha kuwa ametumia nafasi yake kuwawezesha wananchi kunufaika na ufugaji nyuki na kuwataka wafugaji nyuki kuunda vikundi ili waweze kupatiwa mikopo na kufuga kisasa zaidi.
Kwa upande wake, Ofisa nyuki wilayani humo, Costa Mhando, alisema soko la mazao ya nyuki Same bado liko chini kwa sababu wananchi hawana mwamko.
Alisema wilaya hiyo ina wafugaji 1,900 na kuwa kwa mwaka 2008/09 walirina lita 40,000 za asali .
Chanzo: Mwananchi